الكهف
Al-Kahf
The Cave
1 - Al-Kahf (The Cave) - 001
ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ ٱلَّذِيٓ أَنزَلَ عَلَىٰ عَبۡدِهِ ٱلۡكِتَٰبَ وَلَمۡ يَجۡعَل لَّهُۥ عِوَجَاۜ
Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo.
Kuhimidiwa, yaani kusifiwa na kushukuriwa kwa wema, anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye amemteremshia mja wake, Muhammad, hii Qur'ani. Na wala hakujaalia kuwa ndani yake kipo chochote cha dosari, kilicho kwenda kombo na kuacha usawa. Bali ndani yake mna Haki tupu, isiyo na shaka yoyote.
2 - Al-Kahf (The Cave) - 002
قَيِّمٗا لِّيُنذِرَ بَأۡسٗا شَدِيدٗا مِّن لَّدُنۡهُ وَيُبَشِّرَ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ ٱلَّذِينَ يَعۡمَلُونَ ٱلصَّـٰلِحَٰتِ أَنَّ لَهُمۡ أَجۡرًا حَسَنٗا
Kimenyooka sawa, ili kitoe onyo kali kutoka kwake, na kiwabashirie Waumini watendao mema kwamba watapata ujira mzuri.
Na Mwenyezi Mungu ameijaalia Qur'ani imesimama, imenyooka sawa sawa katika mafunzo yake ili kuwaonya wanao kufuru na kukataa, kuwa watapata adhabu kali itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na iwape bishara njema wanao isadiki, ambao wanatenda vitendo vyema, ya kwamba watapata malipo mazuri.
3 - Al-Kahf (The Cave) - 003
مَّـٰكِثِينَ فِيهِ أَبَدٗا
Wakae humo milele.
Malipo hayo ni Pepo watakayo kaa humo milele.
4 - Al-Kahf (The Cave) - 004
وَيُنذِرَ ٱلَّذِينَ قَالُواْ ٱتَّخَذَ ٱللَّهُ وَلَدٗا
Na kiwaonye wanao nena: Mwenyezi Mungu ana mwana.
Na kiwaonye kwa njia makhsusi wale walio msingizia Mwenyezi Mungu kuwa ana mwana, na hali Yeye ametakasika kuwa kama viumbe, akawa mwenye kuzaa au akazaliwa mtoto wake.
5 - Al-Kahf (The Cave) - 005
مَّا لَهُم بِهِۦ مِنۡ عِلۡمٖ وَلَا لِأٓبَآئِهِمۡۚ كَبُرَتۡ كَلِمَةٗ تَخۡرُجُ مِنۡ أَفۡوَٰهِهِمۡۚ إِن يَقُولُونَ إِلَّا كَذِبٗا
Wao hawana ujuzi wa jambo hili, wala baba zao. Ni neno kuu hilo litokalo vinywani mwao. Hawasemi ila uwongo tu.
Wala wao hawana ujuzi wowote wa hayo wala baba zao hawakuwa nao huo. Ni uzushi mkubwa mno huu wa kutoa neno hili vinywani mwao! Wayasemayo ni uzushi, na wala hapana uzushi mkubwa kushinda huu.
6 - Al-Kahf (The Cave) - 006
فَلَعَلَّكَ بَٰخِعٞ نَّفۡسَكَ عَلَىٰٓ ءَاثَٰرِهِمۡ إِن لَّمۡ يُؤۡمِنُواْ بِهَٰذَا ٱلۡحَدِيثِ أَسَفًا
Huenda ukajihiliki nafsi yako kwa ajili yao, kuwasikitikia kwa kuwa hawayaamini mazungumzo haya!
Ewe Nabii! Usijihiliki nafsi yako bure kwa kuhuzunika na kusikitika kwa kuacha kwao kuitikia Wito wako, na kuisadiki hii Qur'ani.
7 - Al-Kahf (The Cave) - 007
إِنَّا جَعَلۡنَا مَا عَلَى ٱلۡأَرۡضِ زِينَةٗ لَّهَا لِنَبۡلُوَهُمۡ أَيُّهُمۡ أَحۡسَنُ عَمَلٗا
Kwa hakika tumevifanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi.
Sisi tumewaumba kwa kheri na shari, na tumevifanya vilio juu ya ardhi ni pambo lake kwa ajili ya manufaa ya watu wake. Hivyo tunawatendea vitendo kama ni mtihani wapate kudhihiri kati yao wenye a'mali njema. Basi aliye pumbazwa na ulimwengu, na asiishughulikie Akhera, huwa amepotea. Na aliye iamini Akhera, huyo huwa ameongoka.
8 - Al-Kahf (The Cave) - 008
وَإِنَّا لَجَٰعِلُونَ مَا عَلَيۡهَا صَعِيدٗا جُرُزًا
Na hakika Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya ardhi kuwa kama nchi ilio pigwa na ukame.
Baada ya kumalizika dunia Sisi tutavifanya vyote vilio juu ya dunia kama ardhi tambarare isio na mimea baada ya kuwa imeamirika kwa mazao ya kijani yenye uhai.
9 - Al-Kahf (The Cave) - 009
أَمۡ حَسِبۡتَ أَنَّ أَصۡحَٰبَ ٱلۡكَهۡفِ وَٱلرَّقِيمِ كَانُواْ مِنۡ ءَايَٰتِنَا عَجَبًا
Bali unadhani ya kwamba wale Watu wa Pangoni na Maandishi walikuwa ni ajabu miongoni mwa ishara zetu?
Walio pumbazwa na starehe za dunia wanakanya kufufuliwa, ilihali hakika ya mambo inathibitisha pana uhai baada ya usingizi mrefu. Na hichi kisa cha Watu wa Pangoni kwenye mlima na bao lilio andikwa majina yao baada ya kufa kwao hakikuwa ni ajabu ya pekee, tukaziacha ishara zote nyenginezo. Ijapo kuwa kisa hicho si cha kawaida, lakini hakikuwa ndio cha ajabu kushinda ishara zetu nyengine zenya kuonyesha uweza wetu.
10 - Al-Kahf (The Cave) - 010
إِذۡ أَوَى ٱلۡفِتۡيَةُ إِلَى ٱلۡكَهۡفِ فَقَالُواْ رَبَّنَآ ءَاتِنَا مِن لَّدُنكَ رَحۡمَةٗ وَهَيِّئۡ لَنَا مِنۡ أَمۡرِنَا رَشَدٗا
Vijana hao walipo kimbilia kwenye pango walisema: Mola wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengezee uwongofu katika jambo letu.
Taja pale walipo kwenda hao vijana kwenye pango, wakafanya hapo ndipo pahali pa kujificha baada ya kukimbia ushirikina na washirikina kuhifadhi Dini yao. Wakasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Tupe maghfira kutoka kwako, na utulinde na adui yetu, na tusahilishie hidaya na tawfiki katika mambo yetu!
11 - Al-Kahf (The Cave) - 011
فَضَرَبۡنَا عَلَىٰٓ ءَاذَانِهِمۡ فِي ٱلۡكَهۡفِ سِنِينَ عَدَدٗا
Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa.
Tukaipokea dua yao hiyo, tukawalaza kwa salama katika hilo pango kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa.
12 - Al-Kahf (The Cave) - 012
ثُمَّ بَعَثۡنَٰهُمۡ لِنَعۡلَمَ أَيُّ ٱلۡحِزۡبَيۡنِ أَحۡصَىٰ لِمَا لَبِثُوٓاْ أَمَدٗا
Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa.
Kisha Mwenyezi Mungu aliwaamsha baada ya kulala kwa muda mrefu, ili matokeo yake yawe ni kudhihirisha ujuzi wetu ni nani katika makundi mawili aliye sibu kukisia muda wa kulala kwao.
13 - Al-Kahf (The Cave) - 013
نَّحۡنُ نَقُصُّ عَلَيۡكَ نَبَأَهُم بِٱلۡحَقِّۚ إِنَّهُمۡ فِتۡيَةٌ ءَامَنُواْ بِرَبِّهِمۡ وَزِدۡنَٰهُمۡ هُدٗى
Sisi tunakusimulia khabari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.
Ewe Mtume! Sisi tunakusimulia khabari zao kweli kweli: Hakika hao walikuwa vijana katika zama zilizo pita ambao walikuwa wameshika Dini ya Haki. Walimuamini Mola wao Mlezi kuwa ni Mmoja tu, na ilihali wamezungukwa na washirikina.
14 - Al-Kahf (The Cave) - 014
وَرَبَطۡنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمۡ إِذۡ قَامُواْ فَقَالُواْ رَبُّنَا رَبُّ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِ لَن نَّدۡعُوَاْ مِن دُونِهِۦٓ إِلَٰهٗاۖ لَّقَدۡ قُلۡنَآ إِذٗا شَطَطًا
Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.
Na tulizithibitisha nyoyo zao juu ya Imani na subira ya kuvumilia shida, pale walipo simama mbele ya watu wao wakasema kwa kujifunga kwa ahadi: Ewe Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye wa Haki, Mola Mlezi wa mbingu na ardhi! Sisi hatumuabudu mungu mwenginewe. Wala hatutoiwacha itikadi hii. Wallahi! Tukisema jenginelo basi itakuwa tunasema lilio mbali kabisa na kweli!
15 - Al-Kahf (The Cave) - 015
هَـٰٓؤُلَآءِ قَوۡمُنَا ٱتَّخَذُواْ مِن دُونِهِۦٓ ءَالِهَةٗۖ لَّوۡلَا يَأۡتُونَ عَلَيۡهِم بِسُلۡطَٰنِۭ بَيِّنٖۖ فَمَنۡ أَظۡلَمُ مِمَّنِ ٱفۡتَرَىٰ عَلَى ٱللَّهِ كَذِبٗا
Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake Yeye. Kwa nini basi hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu?
Kisha wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Hawa watu wetu wamemshirikisha Mwenyezi Mungu. Lau kuwa wameleta hoja iliyo wazi ya kuthibitisha ungu wa hivyo wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Hakika watu hawa ni wenye kudhulumu kwa vitendo vyao hivyo. Wala hapana aliye zidi udhaalimu kuliko mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo kwa kumsingizia washirika.
16 - Al-Kahf (The Cave) - 016
وَإِذِ ٱعۡتَزَلۡتُمُوهُمۡ وَمَا يَعۡبُدُونَ إِلَّا ٱللَّهَ فَأۡوُۥٓاْ إِلَى ٱلۡكَهۡفِ يَنشُرۡ لَكُمۡ رَبُّكُم مِّن رَّحۡمَتِهِۦ وَيُهَيِّئۡ لَكُم مِّنۡ أَمۡرِكُم مِّرۡفَقٗا
Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema yake, na akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu.
Na wakaambiana wao kwa wao: Maadamu sisi tumejitenga nao hao katika ukafiri wao na ushirikina wao, basi kimbilieni pangoni mlinde Dini yenu. Mola wenu Mlezi atakukunjulieni maghfira yake, na atakusahilishieni mambo yenu kwa njia za kukufaeni katika maisha yenu. Haijuulikani kwa hakika ni nani hao Ahlil Kahf, wala zama zao, wala hilo pango lipo wapi walilo kimbilia hao vijana. Pamoja na hayo hapana ubaya kuchunguza, huenda pakapatikana mwangaza japo kidogo juu yake. Ilivyo kuwa Qur'ani Tukufu imetaja kuwa hao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi basi hapana budi kuwa wao na watu wao waliteswa kwa sababu ya Dini, hata wakaona hao vijana wakimbilie pangoni kujificha. Na Taarikhi ya zamani inataja kuwa yalikuwako mateso ya dini katika nchi za Mashariki ya kale yaliyo tokea nyakati mbali mbali. Tutataja katika yafuatayo mateso mawili huenda moja wapo likaelekea na kisa hichi:- Ya kwanza yalitokea zama za mfalme wa Kisaluki, Antiokhus IV, aliye itwa kwa jina la kupanga Nabivanis (kiasi ya 176-84 K.K.). Huyo alipo shika ufalme wa Shamu, na akawa amemili mno kwenye ustaarabu wa Kigiriki na ilimu zake, aliwalazimisha Mayahudi wa Palistina, nayo ilikuwa chini ya Shamu tangu mwaka 194 K.K. washike dini ya Kigiriki, na akavunja sharia zao, na akanajisi Hekalu lao kwa kuweka humo sanamu la Zeus, mungu mkuu wa Magiriki, juu ya madhibahu (kibulani), na kumtolea mihanga ya nguruwe humo. Tena huyo mfalme aliteketeza kwa moto nakla za Taurati zote alizo zipata. Kwa mwangaza huu yaonekana kuwa hawa vijana walikuwa ni Mayahudi, na kwao ni popote katika Palastina, au khasa ni katika Yerusalemu. Na ikawa wakaamka mnamo mwaka 126 B.K. zama za utawala wa Warumi wa Mashariki. Yaani kabla ya kuzaliwa Mtume Muhammad s.a.w. (nako kulikuwa kiasi mwaka 571 B.K.) kwa kiasi ya miaka mia nne na arubaini na tano takriban. Ama mateso ya pili yalitokea zama za Mfalme wa Ufalme wa Kirumi, Hadriatus (117-138). Mfalme huyu aliwatenda Mayahudi kama alivyo watendea Antiokhus tuliye kwisha mtaja sawa sawa. Matokeo ya hayo ni kuwa Mayahudi walitangaza uasi dhidi ya utawala wa Kirumi mwaka 132. Wakawafukuza askari wa ulinzi wa Kirumi, wakaiteka Yerusalemu, na wakatoa sarafu yao ya makumbusho ya ugombozi wa Mji Mtakatifu. Wakashika khatamu za utawala kwa muda wa miaka mitatu. Mwishoni Hadriatus na jeshi lake wakagutuka, wakaushinda uasi, na wakairudisha Palastina chini ya ut'iifu, na wakairudisha Yerusalemu, na wakauvunjilia mbali uwananchi wa Kiyahudi kabisa. Viongozi wa Mayahudi wakauwawa na Mayahudi wakauzwa sokoni kuwa watumwa. Matokeo ya hayo ni kuwa mambo yote ya Kiyahudi aliyapiga marfuku Hadriatus na akapiga marfuku mafunzo ya Kiyahudi na sharia zao. Kwa mujibu wa mwangaza huu wa taarikhi yaonekana kuwa vijana hawa walikuwa ni Mayahudi, na pahala pao ni popote katika Mashariki ya kale, au katika Yerusalemu yenyewe. Yaonekana kuwa waliamshwa mnamo mwaka 435 B.K., yaani kabla ya kuzaliwa Mtume wetu s.a.w. kwa miaka mia na thalathini. Yaonekana kuwa yale mateso ya mwanzo yameelekeana zaidi na kisa hichi cha Watu wa Pangoni, kwa sababu yalikuwa ni ya shida zaidi. Ama mateso ya Kikristo hayaelekeani na kuzaliwa kwa Mtume s.a.w.
17 - Al-Kahf (The Cave) - 017
۞وَتَرَى ٱلشَّمۡسَ إِذَا طَلَعَت تَّزَٰوَرُ عَن كَهۡفِهِمۡ ذَاتَ ٱلۡيَمِينِ وَإِذَا غَرَبَت تَّقۡرِضُهُمۡ ذَاتَ ٱلشِّمَالِ وَهُمۡ فِي فَجۡوَةٖ مِّنۡهُۚ ذَٰلِكَ مِنۡ ءَايَٰتِ ٱللَّهِۗ مَن يَهۡدِ ٱللَّهُ فَهُوَ ٱلۡمُهۡتَدِۖ وَمَن يُضۡلِلۡ فَلَن تَجِدَ لَهُۥ وَلِيّٗا مُّرۡشِدٗا
Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa basi huyo ni mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi.
Na lile pango lilikuwa kwenye mlima, lina nafasi ndani. Lilielekea kaskazini, linapigwa na upepo mzuri. Jua likichomoza muanga wake huwa kuliani mwao, na miale yake huwa mbali nao; na likichwa huwa kushotoni mwao. Kwa hivyo lile jua halipigi ndani ya pango, na kwa hivyo walisalimika na joto la jua, na upepo wa kaskazi unawaingilia. Na yote hayo ni katika ishara za kudra ya Mwenyezi Mungu. Na anaye pata tawfiki ya Mwenyezi Mungu kuokoka basi huokoka, na aliye kosa tawfiki hatopata wa kumwongoa baada yake.
18 - Al-Kahf (The Cave) - 018
وَتَحۡسَبُهُمۡ أَيۡقَاظٗا وَهُمۡ رُقُودٞۚ وَنُقَلِّبُهُمۡ ذَاتَ ٱلۡيَمِينِ وَذَاتَ ٱلشِّمَالِۖ وَكَلۡبُهُم بَٰسِطٞ ذِرَاعَيۡهِ بِٱلۡوَصِيدِۚ لَوِ ٱطَّلَعۡتَ عَلَيۡهِمۡ لَوَلَّيۡتَ مِنۡهُمۡ فِرَارٗا وَلَمُلِئۡتَ مِنۡهُمۡ رُعۡبٗا
Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi tunawageuza kulia na kushoto. Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeli watokea hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu.
Na wewe ukiwaona utadhani wamacho, nao kwa hakika wamelala. Na katika usingizi wao tulikuwa tunawageuza kulia na kushoto mara kwa mara ili kuwahifadhi miili yao isidhurike na ardhi wakafanya madonda. Na mbwa aliye wafuata alinyoosha miguu yake ya mbele mlangoni, naye kalala pia kama kwamba yu macho. Ungeli watokea nao wamo katika hali ile ungeli toka mbio na moyo umejaa khofu kwa walivyo kuwa wanatisha katika kulala kwao. Hapana anaye waona ila atatishika nao. Hayo ili wasikaribiwe na mtu, wala wasiguswe na mtu mpaka wishe muda wao.
19 - Al-Kahf (The Cave) - 019
وَكَذَٰلِكَ بَعَثۡنَٰهُمۡ لِيَتَسَآءَلُواْ بَيۡنَهُمۡۚ قَالَ قَآئِلٞ مِّنۡهُمۡ كَمۡ لَبِثۡتُمۡۖ قَالُواْ لَبِثۡنَا يَوۡمًا أَوۡ بَعۡضَ يَوۡمٖۚ قَالُواْ رَبُّكُمۡ أَعۡلَمُ بِمَا لَبِثۡتُمۡ فَٱبۡعَثُوٓاْ أَحَدَكُم بِوَرِقِكُمۡ هَٰذِهِۦٓ إِلَى ٱلۡمَدِينَةِ فَلۡيَنظُرۡ أَيُّهَآ أَزۡكَىٰ طَعَامٗا فَلۡيَأۡتِكُم بِرِزۡقٖ مِّنۡهُ وَلۡيَتَلَطَّفۡ وَلَا يُشۡعِرَنَّ بِكُمۡ أَحَدًا
Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote.
Kama tulivyo walaza tuliwaamsha wapate kuulizana wenyewe kwa wenyewe wamelala muda gani? Mmoja wao akasema: Umekupitieni muda gani katika usingizi? Wakasema: Tumelala muda wa siku au baadhi ya siku. Walivyo kuwa hawana yakini nayo hayo wakasema: Mwachieni mambo haya Mwenyezi Mungu; kwani Yeye ni Mjuzi zaidi wa haya. Na ende mmoja wenu mjini, na achukue hizi sarafu za fedha achague chakula kizuri kabisa akuleteeni mle. Na awe na mafahamiano mema. Wala mambo yenu yasijuulikane na mtu yeyote.
20 - Al-Kahf (The Cave) - 020
إِنَّهُمۡ إِن يَظۡهَرُواْ عَلَيۡكُمۡ يَرۡجُمُوكُمۡ أَوۡ يُعِيدُوكُمۡ فِي مِلَّتِهِمۡ وَلَن تُفۡلِحُوٓاْ إِذًا أَبَدٗا
Kwani wao wakikutambueni watakupigeni mawe, au watakurudisheni katika dini yao; na hapo hamtafanikiwa kabisa!
Kwani hao watu wakikuoneni watakuuweni kwa kukupopoeni mawe, au watakurejesheeni katika ukafiri kwa nguvu. Nanyi mkirejea ukafirini basi hamtaongokewa kabisa duniani wala Akhera.
21 - Al-Kahf (The Cave) - 021
وَكَذَٰلِكَ أَعۡثَرۡنَا عَلَيۡهِمۡ لِيَعۡلَمُوٓاْ أَنَّ وَعۡدَ ٱللَّهِ حَقّٞ وَأَنَّ ٱلسَّاعَةَ لَا رَيۡبَ فِيهَآ إِذۡ يَتَنَٰزَعُونَ بَيۡنَهُمۡ أَمۡرَهُمۡۖ فَقَالُواْ ٱبۡنُواْ عَلَيۡهِم بُنۡيَٰنٗاۖ رَّبُّهُمۡ أَعۡلَمُ بِهِمۡۚ قَالَ ٱلَّذِينَ غَلَبُواْ عَلَىٰٓ أَمۡرِهِمۡ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيۡهِم مَّسۡجِدٗا
Na namna hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi anawajua vyema. Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao.
Na kama tulivyo walaza na tukawaamsha tulikuja watambulisha kwa watu wa ule mji wapate kujua kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kufufua wafu ni ya kweli. Na Kiyama hapana shaka kitakuja. Watu wa ule mji wakamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Kisha Mwenyezi Mungu akawafisha wale vijana. Watu sasa wakazozana kwa mintarafu yao. Baadhi yao wakasema: Jengeni jengo kwenye mlango wa pango, na tuwaache wao na shani yao. Kwani Mola wao Mlezi anaijua vyema hali yao. Na wakasema wenye kusikilizwa miongoni mwao: Hapa pahala pao tutafanya msikiti kwa sababu ya ibada.
22 - Al-Kahf (The Cave) - 022
سَيَقُولُونَ ثَلَٰثَةٞ رَّابِعُهُمۡ كَلۡبُهُمۡ وَيَقُولُونَ خَمۡسَةٞ سَادِسُهُمۡ كَلۡبُهُمۡ رَجۡمَۢا بِٱلۡغَيۡبِۖ وَيَقُولُونَ سَبۡعَةٞ وَثَامِنُهُمۡ كَلۡبُهُمۡۚ قُل رَّبِّيٓ أَعۡلَمُ بِعِدَّتِهِم مَّا يَعۡلَمُهُمۡ إِلَّا قَلِيلٞۗ فَلَا تُمَارِ فِيهِمۡ إِلَّا مِرَآءٗ ظَٰهِرٗا وَلَا تَسۡتَفۡتِ فِيهِم مِّنۡهُمۡ أَحَدٗا
Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule.
Watasema kikundi fulani katika Watu wa Kitabu (Biblia) wanao jiingiza katika mzozano wa kisa cha Ahlil Kahf (Watu wa Pangoni) kwamba hao walikuwa watatu na wa nne wao ni mbwa wao. Na wengine wanasema: Walikuwa watano, na wa sita wao ni mbwa wao. Tena wengine wanasema: Wao ni saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Waambie hawa wanao khitalifiana: Mola wangu Mlezi ni Mjuzi ambaye hapana wa kumshinda ujuzi wake kuijua idadi yao. Wala hapana wajuao ila watu wachache tu ambao Mwenyezi Mungu amewajuvya hisabu yao. Basi wewe usijadiliane na hao wanao khitalifiana juu ya mas-ala ya hao vijana, ila majadiliano ya juu juu ya upole, bila ya kujaribu kuwakinaisha. Kwani wao hawakinaiki. Wala msimuulize yeyote kati yao juu ya khabari zao. Wewe hakika imekwisha kujia iliyo kweli isiyo na shaka.
23 - Al-Kahf (The Cave) - 023
وَلَا تَقُولَنَّ لِشَاْيۡءٍ إِنِّي فَاعِلٞ ذَٰلِكَ غَدًا
Wala usisema kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho
Wala usiseme kabisa kwa jambo unalo azimia kulendea na kujihimu kulitenda: Mimi nitalifanya hilo baadae!
24 - Al-Kahf (The Cave) - 024
إِلَّآ أَن يَشَآءَ ٱللَّهُۚ وَٱذۡكُر رَّبَّكَ إِذَا نَسِيتَ وَقُلۡ عَسَىٰٓ أَن يَهۡدِيَنِ رَبِّي لِأَقۡرَبَ مِنۡ هَٰذَا رَشَدٗا
Isipo kuwa Mwenyezi Mungu akipenda. Na mkumbuke Mola wako Mlezi pale unapo sahau, na sema: Asaa Mola wangu Mlezi ataniongoa kwenye uwongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.
Ila kusema huko kuambatane na kupenda kwa Mwenyezi Mungu kwa kusema: Inshallah, yaani Mwenyezi Mungu akipenda. Na ukisahau jambo, basi kimbilia kumtaja Mwenyezi Mungu; na useme unapo azimia kufanya jambo na kuliambatanisha na kupenda kwa Mwenyezi Mungu: Huenda Mola wangu Mlezi akaniwafikisha kwenye bora kuliko nililo azimia kufanya, na lenye kuongoka zaidi.
25 - Al-Kahf (The Cave) - 025
وَلَبِثُواْ فِي كَهۡفِهِمۡ ثَلَٰثَ مِاْئَةٖ سِنِينَ وَٱزۡدَادُواْ تِسۡعٗا
Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa.
Na hakika hao vijana walikaa katika pango lao nao wamelala kwa miaka mia tatu, na ikazidi tisa. Aya hii inaonyesha ukweli wa ilimu ya Falaki (Astronomy), nayo ni kuwa ni miaka 300 kwa mwendo wa jua, na miaka 309 kwa hisabu ya mwezi unao fuatwa na Waislamu. Aya hii imeitangulia ilimu ya Falaki.
26 - Al-Kahf (The Cave) - 026
قُلِ ٱللَّهُ أَعۡلَمُ بِمَا لَبِثُواْۖ لَهُۥ غَيۡبُ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضِۖ أَبۡصِرۡ بِهِۦ وَأَسۡمِعۡۚ مَا لَهُم مِّن دُونِهِۦ مِن وَلِيّٖ وَلَا يُشۡرِكُ فِي حُكۡمِهِۦٓ أَحَدٗا
Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa. Ni zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana mlinzi isipo kuwa Yeye, wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.
Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujua zama zao zote. Kwani Yeye Subhanahu ndiye aliye khusika kujua siri za mbingu na ardhi. Jinsi gani kulivyo tukuka kuona kwake kwa viumbe vyote! Na jinsi gani kulivyo tukuka kusikia kwake kwa kila cha kusikilizana! Na hapana katika wa mbinguni na wa katika ardhi wa kuendesha mambo yao isipo kuwa Yeye. Na wala hapana wa kumshiriki katika hukumu yake kiumbe chochote.
27 - Al-Kahf (The Cave) - 027
وَٱتۡلُ مَآ أُوحِيَ إِلَيۡكَ مِن كِتَابِ رَبِّكَۖ لَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَٰتِهِۦ وَلَن تَجِدَ مِن دُونِهِۦ مُلۡتَحَدٗا
Na soma uliyo funuliwa katika Kitabu cha Mola wako Mlezi. Hapana wa kubadilisha maneno yake. Wala nawe hutapata makimbilio isipo kuwa kwake.
Ewe Mtume! Soma uliyo funuliwa kwa wahyi katika Qur'ani. Na katika hayo yamo uliyo funuliwa ya khabari za hao vijana. Wala usisikilize hayo maskhara yao ya kutaka ubadilishe muujiza wa Qur'ani kwa muujiza mwingine. Kwani hakika hapana wa kuyageuza anayo simulia Mwenyezi Mungu maneno ya haki katika miujiza yake. Hakika hapana awezae kubadilisha hayo. Wala usende kinyume na amri ya Mola wako Mlezi, kwani hapo tena hutapata wa kumkimbilia kukuhifadhi naye.
28 - Al-Kahf (The Cave) - 028
وَٱصۡبِرۡ نَفۡسَكَ مَعَ ٱلَّذِينَ يَدۡعُونَ رَبَّهُم بِٱلۡغَدَوٰةِ وَٱلۡعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجۡهَهُۥۖ وَلَا تَعۡدُ عَيۡنَاكَ عَنۡهُمۡ تُرِيدُ زِينَةَ ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَاۖ وَلَا تُطِعۡ مَنۡ أَغۡفَلۡنَا قَلۡبَهُۥ عَن ذِكۡرِنَا وَٱتَّبَعَ هَوَىٰهُ وَكَانَ أَمۡرُهُۥ فُرُطٗا
Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka.
Ewe Mtume! Shikamana na usuhuba wa masahaba wako Waumini, wanao muabudu Mwenyezi Mungu peke yake asubuhi na jioni daima, huku wanataka radhi zake. Wala jicho lako lisiwawache hao kuwaangalia wapinzani wa kikafiri kwa kutaka kustarehe nao katika mapambo ya maisha ya dunia. Wala usikubali kuwafukuza Waumini mafakiri katika baraza yako kwa kumridhisha huyo tuliye mghafilisha moyo wake na kutukumbuka Sisi, kwa kuwa yeye mwenyewe hakuwa tayari kwa hayo, na akawa ni mtumwa wa pumbao lake, na mambo yake katika vitendo vyake vyote hayakufuata njia iliyo sawa. Na anapo katazwa Nabii, basi ndio wanakatazwa wengineo (yaani sote sisi). Na hakika Nabii s.a.w. hataki maisha ya dunia na pumbao lake. Lakini makatazo hayo anaelekezewa Nabii ili wenginewe watahadhari na kutaka pumbao la dunia. Kwani ikiwa yaweza kuwa kwake kutaka pumbao la kimwili, basi kila mwanaadamu yaweza kuwa katika nafsi yake. Kwa hivyo ajilinde.
29 - Al-Kahf (The Cave) - 029
وَقُلِ ٱلۡحَقُّ مِن رَّبِّكُمۡۖ فَمَن شَآءَ فَلۡيُؤۡمِن وَمَن شَآءَ فَلۡيَكۡفُرۡۚ إِنَّآ أَعۡتَدۡنَا لِلظَّـٰلِمِينَ نَارًا أَحَاطَ بِهِمۡ سُرَادِقُهَاۚ وَإِن يَسۡتَغِيثُواْ يُغَاثُواْ بِمَآءٖ كَٱلۡمُهۡلِ يَشۡوِي ٱلۡوُجُوهَۚ بِئۡسَ ٱلشَّرَابُ وَسَآءَتۡ مُرۡتَفَقًا
Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao utawazunguka kama khema. Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyo tibuka. Yatayo wababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno! Na matandiko hayo ya kupumzikia ni maovu mno!
Sema ewe Mtume!: Hakika haya niliyo kuja nayo ni kweli tupu iliyo toka kwa Mola wenu Mlezi. Basi anaye taka kuyaamini na ayaamini. Kwani hiyo ni kheri yake mwenyewe. Na anaye taka kuyakataa na akatae. Kwani huyo haidhulumu ila nafsi yake mwenyewe. Hakika Sisi tumekwisha muwekea tayari anaye jidhulumu nafsi yake kwa ukafiri Moto utao mzunguka kama khema. Na hao walio dhulumu wakiomba wasaidiwe kwa maji huko katika Jahannamu, wataletewa maji kama mafuta yaliyo tibuka yamoto mno, hubabua nyuso kwa uvukuto wake! Kinywaji hicho ni kibaya mno, na Jahannamu ni pahali paovu pa mapumziko yao!!
30 - Al-Kahf (The Cave) - 030
إِنَّ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَٰتِ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجۡرَ مَنۡ أَحۡسَنَ عَمَلًا
Hakika wale walio amini na wakatenda mema - hakika Sisi hatupotezi ujira wa anaye tenda mema.
Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Dini ya Haki uliyo funuliwa wewe, na wakatenda aliyo waamrisha Mola wao Mlezi, nayo ni vitendo vyema, basi Sisi hatuto wapotezea ujira wao wa vitendo vyema walivyo vitenda.
31 - Al-Kahf (The Cave) - 031
أُوْلَـٰٓئِكَ لَهُمۡ جَنَّـٰتُ عَدۡنٖ تَجۡرِي مِن تَحۡتِهِمُ ٱلۡأَنۡهَٰرُ يُحَلَّوۡنَ فِيهَا مِنۡ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٖ وَيَلۡبَسُونَ ثِيَابًا خُضۡرٗا مِّن سُندُسٖ وَإِسۡتَبۡرَقٖ مُّتَّكِـِٔينَ فِيهَا عَلَى ٱلۡأَرَآئِكِۚ نِعۡمَ ٱلثَّوَابُ وَحَسُنَتۡ مُرۡتَفَقٗا
Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati yake. Humo watapambwa kwa mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na at'ilasi, huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri mno ya kupumzikia!
Watu hao watakuwa na Mabustani ambayo watastarehe ndani yake daima dawamu. Kati baina ya miti na majumba yake inapita mito, na watapambiwa yanayo onekana ni ya starehe katika dunia, kama mapambo ya dhahabu, na mavazi yao ni nguo za kijani za hariri za kila namna, wakiegemea juu ya makochi na matakia na mapazia. Watapata malipo bora, na Bustani nzuri ya kudumu na kustarehe. Humo watapata kila wakitakacho.
32 - Al-Kahf (The Cave) - 032
۞وَٱضۡرِبۡ لَهُم مَّثَلٗا رَّجُلَيۡنِ جَعَلۡنَا لِأَحَدِهِمَا جَنَّتَيۡنِ مِنۡ أَعۡنَٰبٖ وَحَفَفۡنَٰهُمَا بِنَخۡلٖ وَجَعَلۡنَا بَيۡنَهُمَا زَرۡعٗا
Na wapigie mfano wa watu wawili: mmoja wao tulimpa vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende, na kati yake tukatia mimea ya nafaka.
Ewe Mtume! Bainisha baina ya hali ya makafiri matajiri na Waumini mafakiri kwa kuwapigia mfano ulio tokea hapo zamani baina ya watu wawili: kafiri na Muumini. Huyo kafiri alikuwa na vitalu viwili vya mizabibu, na tukavizungushia mitende kwa ajili ya pambo na faida pia. Na baina ya hivyo vitalu tukaweka makulima mengine yaliyo stawi na kutoa mazao.
33 - Al-Kahf (The Cave) - 033
كِلۡتَا ٱلۡجَنَّتَيۡنِ ءَاتَتۡ أُكُلَهَا وَلَمۡ تَظۡلِم مِّنۡهُ شَيۡـٔٗاۚ وَفَجَّرۡنَا خِلَٰلَهُمَا نَهَرٗا
Na hivyo vitalu viwili vikitoa mazao yake, wala hapana kitu katika hayo kilicho tindikia. Na ndani yake tukapasua mito.
Na kila kitalu kikawa kinatoa mazao yake kwa wingi na kubaariki. Wala hapana kilicho tindikia. Na tukapasua mto unamiminika kati yao.
34 - Al-Kahf (The Cave) - 034
وَكَانَ لَهُۥ ثَمَرٞ فَقَالَ لِصَٰحِبِهِۦ وَهُوَ يُحَاوِرُهُۥٓ أَنَا۠ أَكۡثَرُ مِنكَ مَالٗا وَأَعَزُّ نَفَرٗا
Naye alikuwa na mazao mengi. Basi akamwambia mwenzake naye akibishana naye: Mimi nimekushinda wewe kwa mali na nguvu za watu!
Na huyo mwenye vitalu alikuwa na mali mengine yenye kutoa mazao yake pia. Basi ikamuingia ghururi kwa neema ile. Katika ile ghururi yake akamwambia mwenzie yule Muumini nao walikuwa wakijadiliana: Mimi nina mali mengi kuliko wewe, na ninakushinda kwa nguvu za jamaa zangu na wasaidizi.
35 - Al-Kahf (The Cave) - 035
وَدَخَلَ جَنَّتَهُۥ وَهُوَ ظَالِمٞ لِّنَفۡسِهِۦ قَالَ مَآ أَظُنُّ أَن تَبِيدَ هَٰذِهِۦٓ أَبَدٗا
Na akaingia kitaluni kwake, naye hali anajidhulumu nafsi yake. Akasema: Sidhani kabisa kuwa haya yataharibika.
Kisha akaingia katika kitalu chake kimojapo pamoja na yule mwenzie Muumini, naye huku amejaa ghururi, akamwambia: Sidhani kabisa kuwa kitalu hichi kitapotea!
36 - Al-Kahf (The Cave) - 036
وَمَآ أَظُنُّ ٱلسَّاعَةَ قَآئِمَةٗ وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيۡرٗا مِّنۡهَا مُنقَلَبٗا
Wala sidhani kuwa hiyo Saa (ya Kyama) itatokea. Na ikiwa nitarudishwa kwa Mola wangu Mlezi, bila ya shaka nitapata marejeo bora zaidi kuliko haya.
Wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na pindi ikawa nikirejea kwa Mola wangu Mlezi kwa kufufuliwa kama unavyo dai wewe, basi Wallahi! Hapana shaka nitapata bustani bora kuliko kitalu hiki huko Akhera. Kwani mimi ni mtu wa neema kwa kila hali. Yeye huyu anakisia hayo ya ghaibu kwa haya yaliyoko sasa. Wala hajui kuwa Akhera malipo yake ni kwa Imani na vitendo vya kheri.
37 - Al-Kahf (The Cave) - 037
قَالَ لَهُۥ صَاحِبُهُۥ وَهُوَ يُحَاوِرُهُۥٓ أَكَفَرۡتَ بِٱلَّذِي خَلَقَكَ مِن تُرَابٖ ثُمَّ مِن نُّطۡفَةٖ ثُمَّ سَوَّىٰكَ رَجُلٗا
Mwenzake akamwambia kwa kubishana naye: Je! Unamkufuru aliye kuumba kutokana na udongo, tena kutokana na tone la manii, kisha akakufanya mtu kaamili?
Mwenzie Muumini akamjibu: Unajiachilia kumkufuru Mola wako Mlezi aliye kuumba tangu asli yako ya Adam kutokana na udongo, kisha kutokana na tone ya maji-maji ya mbegu ya uzazi, kisha akakufanya mtu aliye kamilika? Ikiwa unajiona bora kwa mali yako na jamaa zako, basi mkumbuke Mola wako Mlezi na asli yako ya udongo.
38 - Al-Kahf (The Cave) - 038
لَّـٰكِنَّا۠ هُوَ ٱللَّهُ رَبِّي وَلَآ أُشۡرِكُ بِرَبِّيٓ أَحَدٗا
Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi. Wala simshirikishi na yeyote.
Lakini mimi ninasema: Hakika aliye niumba mimi na akaumba ulimwengu wote huu ni Mwenyezi Mungu Mola wangu Mlezi. Na mimi namuabudu Yeye peke yake, wala simshirikishi na yeyote.
39 - Al-Kahf (The Cave) - 039
وَلَوۡلَآ إِذۡ دَخَلۡتَ جَنَّتَكَ قُلۡتَ مَا شَآءَ ٱللَّهُ لَا قُوَّةَ إِلَّا بِٱللَّهِۚ إِن تَرَنِ أَنَا۠ أَقَلَّ مِنكَ مَالٗا وَوَلَدٗا
Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe,
Na lau kuwa ungeli sema unapo ingia katika hii bustani yako ya duniani na ukaangalia viliomo ndani yake: Haya Mashaallah! Ndio aliyo yataka Mwenyezi Mungu. Wala mimi sina nguvu ya kuyapata haya bila ya msaada wa Mwenyezi Mungu. Hayo inge kuwa ni shukrani za kupelekea kudumu neema yako. Tena akazidi kumwambia: Ikiwa umeniona mimi ni duni kuliko wewe kwa mali na watoto na wasaidizi...
40 - Al-Kahf (The Cave) - 040